Tuesday, April 19, 2016

Mugabe amlalamikia askofu kuhusu ndoa za jinsia moja


Rais Mugabe hupinga sana wapenzi wa jinsia moja

 Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe alikutana na Askofu mkuu wa Canterbury na kuibua maswali kuhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja.

Askofu mkuu Justin Welby amesema alimjibu kiongozi huyo kwamba kuna mitazamo tofauti kuhusu ndoa hizo miongoni mwa waumini wa kanisa la Kianglikana kote duniani.

Aliongeza hata hivyo kwamba wengi wa waumini wanaamini ndoa ni uhusiano wa muda mrefu baina ya mwanamume na mwanamke.

Askofu Welby alisema ni makosa kuwahukumu au kuwaadhibu watu kwa sababu ya msimamo wao kijinsia na kimapenzi.

Hata hivyo, amesema dalili zilionesha Bw Mugabe hakukubaliana naye.

“Sidhani itakuwa haki kusema kwamba Bw Mugabe alikubaliana nami kabisa,” alisema Askofu Welby.

Mkutano huo wa faraghani ulifanyika mjini Harare, baada ya Askofu Welby, ambaye yumo katika taifa jirani la Zambia anakohudhuria mkutano wa viongozi wa kanisa la Kiangilikana kufanya ziara fupi Zimbabwe.

Msemaji wa Lambeth Palace amesema mpango huo ulipangwa dakika za mwishomwisho na ulidumu chini ya saa moja.

Bw Mugabe ni Mkatoliki na hupinga sana ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
Askofu Welby amesema Bw Mugabe hakukubaliana naye kabisa
Maafisa wa kanisa hilo wamesema mkutano huo ulikuwa sana wa kidini badala ya kisiasa ingawa uhusiano baina ya serikali na kanisa ulijadiliwa.

Chanzo BBCswahili

No comments:

Post a Comment