WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepewa
jina jipya la Kisukuma na kukabidhiwa zana nyingine muhimu katika vita ya
kupambana na ufisadi nchini maarufu kwa jina la kutumbua majipu.
Kuanzia juzi, Waziri Mkuu Majaliwa
atakuwa akifahamika kwa jina lingine la Masanja, alilopewa na Wazee wa Kisukuma
wa Lamadi wilayani Busega katika mkoa wa Simiyu. Kabla ya kuwahutubia maelfu ya
wakazi wa Lamadi juzi jioni, wazee hao walimvisha Waziri Mkuu vazi la kijadi la
Kisukuma akiwa katika kigoda, wakamkabidhi usinga, ng’ombe wawili na mkuki
ambao walimueleza kuwa kazi yake ni kuendeleza vita ya ufisadi kwa kuutumia
kutumbua majipu.
“Tunakukabidhi usinga na huu mkuki
utumike kutumbua majipu kwa sababu kazi hii unaifanya vizuri hadi sasa, kwa
hiyo uendelee kutumbua majipu. Na kwa kuanzia sasa, tunakupa jina la kwetu, kwa
sababu wewe ni kijana wetu, utaitwa Masanja,” alisema Mchele Malale kwa niaba
ya wazee wenzake.
Kwa mujibu wa wenyeji, jina la
Masanja lina maana ya kuingia kokote, hali inayomaanisha kuwa Waziri Mkuu
Majaliwa aendelee kutumbua majipu kila mahali. Alipoanza kuhutubia, Waziri Mkuu
alikiri kuwa amepata mapokezi makubwa kwa wananchi wa Lamadi, na zaidi, makubwa
kuliko sehemu nyingi alizokwenda tangu ashike wadhifa wake huo.
“Kwa kweli nimefurahishwa na
mapokezi yenu hapa…tangu nilipotoka Mwanza hadi kufika kwenu (Busega) mapokezi
yamekuwa mazuri, na hapa Lamadi mmetisha. Mmenitia faraja sana,” alisema Waziri
Mkuu na kuongeza: “Lakini nimefurahi kwa zawadi mlizonipa na pia jina jipya la
Masanja.
Nimeandika pale kwenye diary
(shajala) yangu. Mmenipa pia mkuki, mmesema nitumie kama sindano kuendeleza ile
kazi,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wa Lamadi.
Akiwa Bariadi jana, Waziri Mkuu
alisema jina lake sasa ni Masanja Mkusanyaji, na kwamba ataendelea kukabiliana
na wakwepa kodi na mafisadi ili Watanzania wapate huduma stahiki.
Chanzo Habari leo.
No comments:
Post a Comment