WABUNGE wawili, Halima Mdee (Kawe) na Mbunge
wa Ukonga, Mwita Waitara na wanachama wengine wa Chadema wamepandishwa
kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Theresa Mmbando.
Wengine waliopandishwa ni Diwani wa
kata ya Saranga, Kinondoni, Ephraimu Kinyafu pamoja na mwanachama wa Chadema,
Rafii Juma.
Watu hao walipandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Mwenyekiti wa wabunge na madiwani wa Ukawa, Manas
Mjema ambaye pia anakabiliwa na mashitaka hayo hakufika mahakamani hapo.
Washitakiwa walifikishwa mahakamani
jana mchana wakiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, wakitoka Kituo Kikuu
Kanda ya Dar es Salaam.
Akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali,
Mwaanamina Kombakono alidai kuwa Februari 27, mwaka huu katika Viwanja vya
Karimjee Dar es Salaam, kwa pamoja washtakiwa walimjeruhi Mmbando na
kumsababishia majeraha mbalimbali kwenye mwili wake.
Washitakiwa walikana mashitaka, na
upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo wanaomba
tarehe nyingine ya kutajwa. Pia waliiomba mahakama itoe hati ya mwito wa kuitwa
Mjema kutokana na kitendo chake cha kutofika mahakamani.
Chanzo Habari Leo.
No comments:
Post a Comment