UTABIRI wa Hali ya Hewa kwa mvua za masika
zinazoanza wiki hii nchini umeonesha zitakuwa za wastani hadi juu ya wastani
katika maeneo mengi ya nchi huku baadhi ya sehemu zikiwa chini ya wastani.
Mvua hizo za masika katika kipindi
cha Machi hadi Mei mwaka huu , zinatarajiwa kuanza wiki hii katika mikoa ya
Kagera na Mara na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) Dk Agness Kijazi alisema hayo jana wakati akitoa utabiri wa
hali ya hewa nchini. Alisema katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda
za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na maeneo machache ya mikoa ya Tanga na
Kisiwa cha Pemba, mvua zitanyesha hadi juu ya wastani.
“Maeneo mengi ya nchi hususan Nyanda
za Juu Kusini Magharibi mwa nchi, Kanda ya Kati na Pwani ya Kusini, yanatarajia
kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani,” alisema Dk Kijazi.
Alisema katika mikoa ya Dar es
Salaam , Pwani na Morogoro na Kusini Magharibi mwa mkoa wa Tanga zitakuwa za
wastani hadi chini ya wastani huku Kilimanjaro, Arusha na Manyara mvua zitaanza
wiki ya pili ya mwezi huu na zitakuwa za wastani na juu ya wastani.
Dk Kijazi alisema mvua hizo za msimu
kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua zilianza Novemba mwaka jana na
zitaendelea hadi Aprili mwaka huu. Alisema zitakuwa za wastani hadi chini ya
wastani katika maeneo mengi.
Alitaja mikoa inayohusika ni ya
Kanda ya Magharibi ambayo ni Kigoma, Tabora , Katavi na Rukwa. Mingine ni ya
Kanda ya Kati; Singida na Dodoma pamoja na mikoa ya Mbeya, Songwe ,Iringa,
Njombe na Kusini mwa Morogoro pamoja na Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Dk Kijazi alisema katika msimu huo
wa mvua, pia inatarajiwa kuwapo upepo mkali kwa baadhi ya maeneo ya nchi
yatakayopata mvua hizo za masika. Alisema TMA inashauri watumiaji wa taarifa za
hali ya hewa wakiwamo wakulima, wafugaji, mamlaka za Wanyamapori, mamlaka za
Maji na Afya kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa hali ya hewa.
Chazo Habari Leo.
No comments:
Post a Comment